Saturday, 14 February 2015

VPL kuendelea kunguruma leo,Coastal na Mbeya.

Ligi kuu soka Tanzania inaendelea kunguruma leo katika viwanja mbalimbali.

Mtibwa sukari watacheza na Ndanda,huku Mbeya City wakialikwa na Coastal Union ya Tanga vilevile Mgambo ya Tanga watacheza na Stendi United ya Shinyanga.

Kuelekea mechi hizo Timu ya Coastal Union ya Tanga imesema kuwa itahakikisha inapambana vilivyo ili kuweza kuhakikisha inachukua pointi tatu muhimu dhidi ya Mbeya City kwenye mpambano utakaopigwa leo kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani.

Coastal Union itangia kwenye mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi yao ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye uwanja wa sokoine jijini Mbeya ambapo Mbeya City iliweza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ambalo lilipatikana kwa njia ya penati.

Akizungumza maandalizi ya kuelekea mchezo huo,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga alisema kuwa maandalizi ya kuelekea mechi hiyo imekamilika kwa asilimia kubwa kwa kufanya mazoezi asubuhi na jioni.

Amesema kuwa mipango yake mikubwa ni kuhakikisha wanafuta machungu ya kufungwa na Yanga bao 1-0, kwenye mechi yao ya Ligi kuu iliyochezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani jambo ambalo halikuwafurahisha mashabiki na wapenzi wa soka.

Aidha amesema kutokana na kikosi chake kuendelea kuimarika kila mchezo wanaokuwa wakicheza wana matumaini makubwa ya kupata ushindi ambao utawawezesha kusogea kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.

Alisema kuwa ligi kuu msimu huu imekuwa ni ngumu sana lakini kubwa ni kujipanga hivyo wamejipanga vizuri kwa umakini mkubwa lengo likiwa kukiwezesha kikosi hicho kinapata matokeo mazuri.

Mwisho.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO COASTAL UNION.

0 comments:

Post a Comment