Monday, 5 May 2014

Baada ya kubeba ubingwa Conte asifiwa na Juve



Juventus walimsifu sana kocha wao  Antonio Conte kwa kushinda taji la tatu la Serie A, baada ya kufufua klabu hiyo kufuatia kashfa ya kupanga mechi, kushushwa ngazi hadi ligi ya daraja la pili na kukosa kufuzu kwa michuano ya Ulaya.
Kocha huyo mwenye  miaka 44, ambaye majuzi alijibizana vikali na kocha wa zamani wa Juve Fabio Capello, meneja wa Italia Cesare Prandelli, Rudi Garcia wa Roma na Rafael Benitez wa Napoli, ameifufua Juventus ambayo hujulikana kwa utani kama Bibi kizee, tangu atue huko 2011.
"Conte aliingiza imani yake kwenye kikosi siku yake ya kwanza huko, shukrani zake nyingi zinafaa kumwendea kwani ni tukio la kihistoria,” alisema mkurugenzi Giuseppe Marotta  akizungumza na Sky Sport .
Juventus walitwaa taji Jumapili bila hata kucheza mchezo  baada ya AS Roma, timu pekee ambayo ilikuwa na nafasi ya kushindana nao, kushindwa 4-1 dhidi ya Catania.
Kabla ya Conte kutua huko, Juventus walikuwa bado wanahangaika baada ya kashfa ya upangaji mechi ambayo ilipelekea wao kupokonywa mataji ya 2005 na 2006 na kushushwa ngazi hadi Serie B.
Walikuwa wamemaliza ligi ya nyumbani wakiwa nambari saba kwa misimu miwili mfululizo kabla ya kuteuliwa kwake na hawakucheza michezo ya Ulaya msimu wake wa kwanza akiwa kwenye usukani, lakini sasa wanasherehekea kushinda taji lao la 30 baada ya kushinda mara tatu mfululizo.
Kipa Gianluigi Buffon alisema wakati muhimu kwao katika kampeni yao ya kuwania ubingwa ulikuwa ushindi wao wa 1-0 dhidi ya Genoa mwezi Machi baada ya mpira wa adhabu wa  Andrea Pirlo kuwakabidhi ushindi kukiwa na dakika mbili zilizokuwa zimesalia za mchezo huo.

0 comments:

Post a Comment