Miyeyusho amtwanga Matumla
BONDIA Francis Miyeyusho ameendeleza ubabe baada ya usiku huu kumshinda kwa pointi Mohamed Matumla katika pambano lisilo la ubingwa uzito wa Bantam, ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam.Mtoto wa Rashid Matumla alimaliza raundi 10 za pambano na majaji wote watatu wakampa ushindi wa pointi Chichi Mawe- ambao alistahili,imeripotiwa na Binzubeiry
Pamoja na kushinda, Miyeyusho alikutana na mpinzani mkali ulingoni ambaye alisimama naye wakijibizana makonde mwanzo hadi mwisho.
Chichi alianza vizuri pambano hilo akimkalisha chini mpinzani wake raundi ya kwanza tu, baada ya kumpa ngumi ya kidevu ya kushitukiza.
Hata hivyo, Matumla aliinuka na kumalizia vizuri raundi hiyo, kisha kuibuka upya katika raundi ya pili na kuendelea vizuri hadi mwisho.
Miyeyusho alipiga ngumi nyingi zaidi ya mtoto wa Matumla, aliyeongozwa na baba yake ulingoni lakini mabondia wote walichapana makonde ya nguvu na kila mmoja kuna wakati alionekana kulewa.
Pambano hilo lilitawaliwa na vurugu za mashabiki wa mabondia hao kutokana na upinzani wa asili- Matumla akikusanya watu wa Keko na Temeke kwa ujumla na Miyeyusho akikusanya watu wa Kinondoni na Manzese.
Miyeyusho alipanda ulingoni leo kiasi cha wiki tatu tangu apigwe vibaya na Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand Aprili 19 kwenye ukumbi huo huo kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya kwanza sekunde ya 55.
Awali, Miyeyusho alimpiga baba yake mdogo Matumla, Mbwana Matumla Oktoba 30, mwaka 2011 na leo ameendeleza ubabe dhidi ya ukoo huo maarufu katika mchezo wa ngumi.
Hilo lilikuwa pambano la 51 kwa Miyeyusho tangu aanze kupigana kifua wazi Februari 1, mwaka 1998 akiwa ameshinda mapambano 38, kati ya hayo 23 kwa KO na kupigwa 11, kati ya hayo 10 kwa KO na sare mawili.
Mtoto wa Rashid Matumla ambaye ngumi katika ukoo wao zinaanzia kwa babu yake Mzee Ally Matumla, leo amepigwa kwa mara ya kwanza katika pambano la 15 tangu ajitose kwenye ngumi za kulipwa Novemba 17, mwaka 2010 akiwa ameshinda mapambano 11, manne kwa KO na ametoka sare mara tatu.
Taarifa hizi zimetolewa kutoka Binzubeiry
0 comments:
Post a Comment