Sunday, 11 May 2014

Tanzania na Nigeria leo kuelekea Senegal

Mei 11 2014.
Mashindano ya CAF kwa Vijana wa chini ya Miaka 20 itaendelea kurindima tena leo ambapo  Tanzania yaani  Ngorongoro Heroes itapambana na Nigeria yaani Flying Eagles.
Ngorongoro Heroes, ambayo katika Raundi ya Kwanza iliitoa Kenya kwa Penati 4-3 baada ya kwenda Sare katika Mechi mbili, ipo chini ya Kocha John Simkoko na Msaidizi wake Mohamed Ayoub, lakini wana kibarua kigumu kwani Nigeria ndio wenye Rekodi kwenye michuano hii kwa kutwaa Kombe hili mara 6 wakifuatiwa na Egypt waliolitwaa mara 4.
Kwa niaba ya wachezaji wenzake, mlinda mlango namba moja na nahodha wa timu hiyo Aishi Manula amewaomba wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika mchezo huo. Waamuzi watakaochesha pambano hili hii leo  la Ngorongoro Heroes watatoka Congo na kuongozwa na Jean-Jacques Ndala Ngambo atakayesaidiwa na Oliver Safari Kabene, Nabina Blaise Sebutu na Mupemba Ignace Nkongolo.
Kamishna wa Mechi ni Poiret Antoine Ralph Danny kutoka Shelisheli.
Mechi za Marudiano za Raundi hii zitachezwa Wikiendi ya Mei 23 hadi 25.
Fainali za Mashindano haya zitachezwa Nchini Senegal kuanzia Machi 8 hadi 22 Mwaka 2015 na Timu zitakazotinga Nusu Fainali zitaiwakilisha Afrika kwenye Kombe la Dunia, 2015 FIFA U-20 World Cup, huko Nchini New Zealand.

0 comments:

Post a Comment