Tutatisha nikiwa na Messi kombe la dunia-Aguero
Mchezaji wa Manchester City ya Uingereza, Sergio Aguero amesema kwamba yuko fiti na tayari kwa ushirikiano na nyota wa FC Barcelona ya Hispania Lionel Messi, kuongoza jaribio la timu ya taifa ya Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Brazil,Imeelezwa na Goal.comAguero alikuwa na msimu mbaya wa michuano ya ndani Uingereza kutokana na jinamizi la majeraha, lakini alifanikiwa kupachika jumla ya mabao 28 katika mechi 34, na ingawa alikosa mechi muhimu za kuamua hatima ya Man City katika taji la Ligi Kuu, alirudi kikosini Mei 11 siku ya kufunga msimu.
Wakati hofu ikizingira kuhusu utayari wake kuelekea fainali hizo zinazoanza Juni 12, Aguero ameibuka na kubainisha ndoto ya kuunda pacha hatari na nyota mwenzake huyo anayekipiga Nou Camp, ambaye anamtaja kwamba atakuwa mhimili wa kikosi chao kutwaa ubingwa katika ardhi ya mahasimu wao Brazil.
“Nilicheza mechi ya kufunga msimu nikiwa na klabu yangu na tangu hapo kwa sasa ninasubiri kupigania heshima ya Argentina katika fainali za Kombe la Dunia.
Itakuwa nafasi kubwa na muhimu kucheza katika michuano mikubwa nchini Brazil,” alifichua Aguero.
Alipoulizwa kama anahisi Argentina inaweza kutwaa ubingwa, Aguero alijibu: “Ndiyo, kwanini isiwe? Tuna Lionel Messi, mchezaji bora zaidi kwa sasa katika uso wa dunia, akiwa ndani ya kikosi chetu. Alituongoza sisi kuwa vinara kufuzu fanali hizi kutokea kanda ngumu (Amerika Kusini).
“Tuna safu kali ya ushambuliaji inayomhusisha pia (Ezequiel) Lavezzi na kimsingi nitajaribu kadri iwezavyo kufunga mabao, huku tukiwa na safu nzuri zaidi ya kiungo wa kutusapoti sisi. Tuna vipaji na nyota wenye uwajibikaji kuweza kukichapa kikosi chochote,” alisisitiza Aguero.
Wakati wengi wakiamini kuwa Argentina imepangwa kundi jepesi la E, Aguero anaonesha kulihofia kundi lake kwa kupinga si jepesi: “Watu wanasema tuko katika kundi nyanya, lakini nani anajua watakuwaje wapinzani wetu?.”
Aguero amesema kuna nchi kama Bosnia na Hezgovina,Iran na Nigeria na kusema kuwa Nigeria ni mabingwa wa Afrika kwa hiyo hawezi kuwabeza ilhali Iran inacheza soka la Kuvutia.
0 comments:
Post a Comment