Yanga kuwasilisha muhtasari wa mkutano TFF
UONGOZI wa klabu ya Yanga, umesema utawasilisha muhtasari wa mkutano wao mkuu wa Juni Mosi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baada ya kukamilisha taratibu zake.Yanga ilifanya mkutano wake mkuu katika Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, ambako mbali na kufanya marekebisho ya katiba kama walivyoagizwa na TFF, pia waliamua mambo mbalimbali ikiwamo kumuongezea mwaka mmoja madarakani mwenyekiti na makamu wake, jambo ambalo lilizua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama wakidai katiba inasiginwa.
Kutokana na hali hiyo, wanachama hao walijiorodhesha majina na kuwasilisha TFF malalamiko yao wakipinga uamuzi wa wenzao kwa madai ya kuvunjwa kwa katiba ya klabu hiyo.
Juzi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura, alikiri shirikisho hilo limepokea malalamiko kuhusu uamuzi uliofanywa na mkutano mkuu wa Yanga uliofanyika Juni Mosi, mwaka huu.
“Hivyo, tunasubiri muhtasari wa mkutano huo kutoka kwa uongozi wa Yanga, ili tuweze kutoa mwongozo kama ikibidi,” alikaririwa Wambura katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto, alisema wana taratibu zao za kufanya kazi katika taasisi yao, hivyo muhtasari huo watauwakilisha hivi karibuni, kwani hakuna sheria inayosema unatakiwa uwasilishwe ndani ya muda fulani.
Chanzo;Tanzania daima
0 comments:
Post a Comment