Nyota Copa Coca-Cola warejea
NYOTA wawili waliochaguliwa kwenda kwenye kambi ya kimataifa ya Copa Coca-Cola iliyofanyika nchini Brazil wiki iliyopita, wamerejea nchini juzi usiku.Wachezaji hao, Ali Mabuyu kutoka Ilala na Juma Yusuf wa Zanzibar, walipokelewa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), na viongozi wa Kampuni ya Coca-Cola Kwanza Tanzania na wadau mbalimbali wa soka hapa nchini.
Katika ziara hiyo ya mafunzo, vijana hao pia walishuhudia mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia kati ya Brazil na Croatia.
Wakizungumzia kuhusu kambi hiyo iliyofanyika katika Jiji la Sao Paulo, Mabuyu na Yusuf, walisema wamejifunza mbinu mbalimbali za soka, nidhamu ya mchezo ndani na nje ya uwanja na kumiliki mpira.
Mabuyu alikuwa mchezaji bora wa michuano ya Copa Coca-Cola 2013 kutoka timu ya soka ya vijana chini ya miaka 15 ya Mkoa wa kisoka wa Ilala na Yusuf ni mfungaji bora wa michuano hiyo kutoka timu ya Mjini Magharibi, hivyo walipata nafasi hiyo kama sehemu ya kujifunza.
Wakiwa katika kambi hiyo ya mafunzo ya kimataifa, vijana hao walifanikiwa kupata tuzo mbalimbali, vikiwemo vikombe, medali, vyeti vya ushiriki na mipira iliyosainiwa na wachezaji wa zamani wa soka nchini Brazil.

0 comments:
Post a Comment