Sunday, 13 July 2014

Marwa, Sakilu watesa mbio za taifa,Tabora wajikongoja.

Wanariadha Dickson Marwa na Jackline Sakilu, wameibuka washindi wa mbio za taifa mwaka huu katika mita 10,000 na 5,000 zilizoanza kutimua vumbi jana katika Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.
Dickson akiwakilisha Mkoa wa Mara na Jackline Sakilu Mkoa wa Arusha, waliibuka washindi, wakikimbia kwa muda wa dakika 28:30.22 na 15:58.63.
Kabla ya kuanza kwa mbio hizo majira ya asubuhi, wanariadha waliomboleza kwa dakika moja kifo cha aliyekuwa Ofisa wa Jeshi la Polisi na kiongozi wa zamani wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), ACP Ernest Saria (69) aliyefariki dunia usiku wa Jumanne wiki hii nyumbani kwake Pugu, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui aliongoza tukio hilo ambapo alisikika akisema marehemu Saria atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kuinua riadha nchini.
Nafasi ya pili, katika mita 10,000 wanaume ilishikwa na Joseph Teofil (Arusha) akikimbia kwa dakika 28:32.33, na Elia Daudi (Dodoma) alishika nafasi ya tatu akitumia muda wa dakika 28:35.07
Gabriel Gerald na Fabian Nelson (wote Kilimanjaro) waling’ang’ania nafasi za 4 na 5 wakifukuza upepo kwa dakika 28:41.87 na 28:59.96.
Mkoa wa Kagera ulishika nafasi ya sita katika mbio hizo, ambapo Pascal Mombo alikimbia kwa muda wa dakika 29:15.25.
Sakilu akikimbia mita 5,000 wanawake kwa muda wa dakika 15:58.63, akiwapiku wanariadha wenzake kutoka Arusha; Failuna Abdi (dk. 16:00.59) na Catherine Lange (dk. 16:28.85).
Magdalene Chrispine akiwakilisha Mkoa wa Kagera alishika nafasi ya nne akikimbia kwa muda wa dakika 17:21.25 huku Anna Joseph (Kagera) akibanwa mbavu na kushika nafasi ya nane kwa muda wa dakika 20:48.35.
Mkoa wa Tabora mita 5,000 wanawake, umeshika nafasi za tano, saba na tisa ukiwakilishwa na Eunice Musa (dk. 18:27.26), Upendo Moses (dk. 20:45.82) na Pendo Stanlaus (dk. 20:52.28).

0 comments:

Post a Comment