Monday, 14 July 2014

Tuzo ya Messi ni aibu asema Collymore.

Jana Argentina ilichapwa Bao 1-0 na Ujerumani kwenye Fainali ya Kombe la Dunia na Kombe kwenda Ujerumani  lakini Nahodha wao Lionel Messi alizoa Mpira wa Dhahabu, ikimaanisha yeye ndio alikuwa Mchezaji Bora wa Fainali za Kombe la Dunia zilizochezwa Brazil.
Mbali ya Messi kutwaa Tuzo hiyo, wengine waliozoa Tuzo binafsi kwenye Fainali hizo ni mshambuliaji wa Colombia, James  Rodriguez, aliyetwaa Buti ya Dhahabu kwa kuwa Mfungaji Bora, Kipa wa Ujerumani, Manuel Neuer, aliyetwaa Glovu ya Dhahabu na Paul Pogba wa Ufaransa alietunzwa kama Mchezaji Bora Kijana.
Lakini baadhi ya Wachambuzi wamekuja juu na kudai kumpa Mpira wa Dhahabu Messi ni ‘aibu kubwa.’
Wengi walishangazwa na uteuzi huo wa FIFA wakidai Messi, mwenye Miaka 27, alionekana mchovu na chini ya kiwango kwenye Mechi nyingi za Mashindano hayo huko Brazil.
Mmoja wa Wachambuzi hao, Stan Collymore, Mchezaji wa zamani wa Liverpool amesema  Messi, licha ya kufunga mabao 4 kwenye Fainali hizo na kuisaidia kuifikisha Timu yake Fainali, hakustahili na wapo wengi walifaa kupewa Tuzo hiyo.
Collymore alisema: “Kwenye Fainali uchezaji wake ulikuwa hafifu. Tumemwona mara 3 au 4 sasa akicheza ovyo chini ya kiwango ukiondoa ya Mipira miwili au mitatu aliyokokota na kukimbia nayo!”
Aliongeza: “Hii ni aibu kubwa kumpa yeye Mpira wa Dhahabu. Ukiwaangalia Wachezaji kama James Rodriguez, au hata Mchezaji wa Chile Alexis Sanchez na Manuel Neuer, wao wanastahili zaidi!”
Alimalizia: “Hata kwenye mchezo wa  Fainali  hakuwa Mchezaji Bora wa Argentina, kwangu Kura inakwenda kwa Javier Mascherano!”

0 comments:

Post a Comment