Baada ya suluhu ya Mtwara,Simba kurudi Zanzibar.
Kikosi cha Simba chini ya Kocha Mkuu Mzambia, Patrick Phiri, kinatarajiwa kuondoka jijini Dar es Salaam leo kwenda Zanzibar kwa maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania bara itakayoanza Jumamosi hii.Simba mabingwa mara 18 wa ligi ya Bara tangu mwaka 1965, itaanza kampeni ya ligi hiyo kwa kuwakaribisha Coastal Union ya Tanga, mabingwa wa ligi hiyo mwaka 1988.
Kwa mujibu wa Makamu Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, kikosi chao kinaondoka leo jijini Dar es Salaam kwenda Zanzibar kikiwa na nyota wake wote.
Kaburu alisema timu hiyo itaendelea kujifua visiwani Zanzibar na itarejea jijini Dar es Salaam siku moja kabla ya kuwakabili Coastal Union katika uwanja wa Taifa.
Aidha, Kaburu alisema, wana imani kubwa na kikosi chao licha kufungwa bao 1-0 na URA ya Uganda katika mechi ya kirafiki iliyochezwa Ijumaa katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na suluhu ya bila kufungana na Ndanda FC.
Simba wanarejea Zanzibar baada ya kucheza mechi tatu za kirafiki; wakiifunga Gor Mahia ya Kenya (3-0) kabla ya kufungwa 1-0 na URA kisha juzi kutoka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara.
0 comments:
Post a Comment