Wednesday, 31 December 2014

FDL Rhino na Geita Sports kupambana leo hapa Tabora.

Klabu ya Rhino Rangers ya hapa mkoani Tabora itashuka dimbani leo kupambana na Geita Gold uwanja wa Ali Hassan Mwinyi katika mwendelezo wa ligi daraja la kwanza FDL.

Akizungumza na mtandao huu kocha msaidizi wa Rhino Didas Kunde amesema kuwa wamejiandaa vya kutosha kuelekea mpambano huo kilichobaki ni vijana wake kufanya kazi.

Didas amesema kuwa katika mchezo uliopita wao wamehesabu kama wamefungwa na leo watahakikisha kushinda ili wajiweke katika nafasi nzuri.

Katika mchezo uliopita Rhino ilitoka sare ya 1-1 na Polisi Mara mchezo uliopigwa katika uwanja wa Mwinyi.

Geita Gold Sports walitoka 0-0 dhidi ya Burkinafaso katika mchezo  uliopita, mjini Morogoro.
Kwa upande wa Geita kupitia kwa Msemaji wao Telu Mpeka Yusuph alisema wameshukuru kupata pointi moja katika mchezo wao na Burkinafaso Jumamosi iliyopita kwa kuwa mchezo ulikuwa mgumu kutokana na uwezo wa wapinzani wao.
Yusuph alisema walistahili kupata pointi hiyo ugenini kwa kuwa wenyeji wao walikuwa wamejipanga kushinda.

Ameongeza kuwa  wanahitaji pointi tatu ili waweze kujiweka katika mazingira mazuri ya kugombania kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Timu hizi zipo Kundi B ambalo linaongozwa na Mwadui FC yenye pointi 25 ikifuatiwa na Toto African na JKT Oljoro zenye pointi 22 kila mmoja huku Polisi Tabora ikiwa na alama 20.

0 comments:

Post a Comment