Wednesday, 4 February 2015

Duh...Hali halisi ya Uwanja wa Mwinyi,usafi kuanza muda wowote.

Uongozi wa  Uwanja wa ALI HASSAN  MWINYI  MKOANI TABORA umewatoa hofu wapenzi na washabiki wa soka mkoani hapa kuhusu suala la usafi wa uwanja huo.

Akizungumza na mtandao huu Meneja wa uwanja huo bwana HAMIS MOURAD amesema kuwa usafi katika uwanja huo utaanza muda wowote hadi kufikia siku ya ijumaa.

Mourad amesema kuwa ingawa wanapata mapato kupitia ligi daraja la kwanza na ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa bado pesa za kuweka sawa hali ya usafi na ukarabati haitoshi.


Kauli hiyo imekuja baada ya vilabu vinavyoshiriki ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa kulalamikia hali ya uwanja huo huku ikionekana kuwa nyasi za uwanja huo zimekuwa ndefu katika baadhi ya maeneo na pia sehemu ya katikati ya uwanja kuharibiwa na maji.

Katika hatua nyingine Mourad ameeleza kuwa iwapo mtu yeyote anahitaji kutumia uwanja lazima aonane na viongozi husika ili kuimarisha ulinzi wa vifaa.

Mourad amesema kuwa ni marufuku kwa mtu kwenda kuingia uwanjani bila ruhusa maalumu kutoka kwa uongozi.
Mtandao huu umeshuhudiwa pindi mvua zikinyesha sehemu ya katikati ya uwanja huwa maji yanasimama na kuleta adha kwa wachezaji.

Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi ulijengwa mwaka 1988 wakati wa utawala wa Chama Kimoja chini ya Uongozi wa Rais wa Pili wa Tanzania Mh. Ally Hassan Mwinyi.

Historia inasema ujenzi wa uwanja huo ulitokana na Wananchi kuchangia nguvu zao kiihari na hata kilazima mpaka Uwanja ulipokamilika kwa ahadi kwamba uwanja huo ni wa kisasa na itakua chanzo kikubwa cha mapato kwa Mkoa.

Ikimbukwe kuwa mwaka jana Uwanja huu ulifungwa na TFF baada ya sehemu ya uwanja kutumika kama darasa lakini baadaye uliruhusiwa baada ya darasa hilo kuondolewa.

0 comments:

Post a Comment