Tuesday, 3 February 2015

Luis Figo apenya kugombea urais FIFA,kupambana na akina Blatter.

Shirikisho la soka duniani  FIFA imethibitisha kuwa Rais  Sepp Blatter atagombea Urais kwa Kipindi kingine cha Miaka Minne akisimama pamoja na Wagombea wengine Luis Figo, ambaye ni mshambuliaji  wa zamani wa Ureno, Rais wa shirikisho la Uholanzi Michael van Praag na Mwana Mfalme wa Jordan, Ali Bin Al-Hussein.

Bodi ya Utawala ya FIFA imetamka kuwa Wagombea hao Wanne watapitia kwenye tathmini ya Kimaadili kabla hawajathibitishwa kama Wagombea.

Mgombea mmoja, Jerome Champagne, wa Ufaransa, alijitoa licha ya kutangaza kugombea baada ya kushindwa kupata Udhamini wa Vyama Vitano vya Soka vya Nchi Wanachama wa FIFA kama taratibu za Uchaguzi zinavyotaka.

Blatter, mwenye Miaka 78, anawania Urais kwa Mara ya 5 tangu atwae wadhifa huo Mwaka 1998 na anatarajiwa kushinda tena kwenye Uchaguzi utakaofanyika Mjini Zurich, Uswisi Mei 29 Mwaka huu.

Blatter anapingwa Nchi za Ulaya, hasa baada ya Uingereza  kubwagwa katika azma yake ya kuwa Mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2018 na 2022 ambazo wamepewa Urusi na Qatar, Blatter anatarajiwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa FIFA.

Blatter anategemewa kuzoa Kura toka Asia, Afrika na Marekani ya Kusini ambao ndiko waliko Wanachama wengi wa FIFA ukilinganisha na 53 wa Ulaya kati ya Wanachama 209 Duniani.

0 comments:

Post a Comment