Thursday, 2 April 2015

Pluijm asema hawajabweteka na ushindi wa 5-1

Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema kwamba hatabweteka kwenye mechi yao ya marudiano dhidi ya Platinum ya Zimbabwe pamoja na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 nyumbani.
 
Pluijm alisema kwamba wachezaji wake watatakiwa kuwa katika kiwango chao kwa asilimia mia moja ili kuitoa timu hiyo ya Zimbabwe na kukata tiketi ya kuingia raundi ya pili ya mashindano Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha huyo amesema Wachezaji wako katika morali ya hali juu na kuongeza kuwa wamefanya maandalizi ya kutosha mpaka sasa, wachezaji wamedhamiria na wamefanya bidii kubwa mazoezini.
Pluijm ameongeza kuwa wachezaji wote isipokuwa Kpah Sherman na Andrey Coutinho wako kwenye hali nzuri kuelekea mchezo huo utakaopigwa keshokutwa.

Yanga inaelekea Zimbabwe ikiwa na faida ya mabao 5-1 iliyopata nyumbani dhidi ya Platinum ya Zimbabwe na hivyo inahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote kusonga mbele kwenye hatua inayofuata.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya kimataifa walifika hatua hiyo baada ya kuitoa timu ya BDF ya Botswana ambapo kwenye mchezo wa awali uliochezwa Dar es Salaam waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 kabla ya kufungwa kwa mabao 2-1 kwenye mchezo wa marudiano uliochezwa Gaborone, Botswana na Yanga kufuzu kwa faida ya bao la ugenini.
Chanzo Habari leo

0 comments:

Post a Comment