Tuesday, 29 April 2014

Ukarabati uwanja wa Sokoine unaendelea



Ukarabati wa vyoo katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya ikiwa ni maandalizi ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na Malawi ‘The Flames’ utakaopigwa Mei 4, mwaka huu, uko hatua za mwisho.
Akizungumzia hilo Meneja wa Uwanja wa Sokoine, Modestus Mwaruka, alisema kuwa kazi ya ukarabati wa vyoo katika uwanja huo imeshakamilika licha ya kuwa kazi haikuwa rahisi kutokana na ugumu wa zege lililojengewa awali.
Meneja huo alisema kuwa kazi imefanywa na Kampuni ya ujenzi ya Mayuma Company ya jijini humo na ilitakiwa kukamilika Aprili 30.
Mwaluka alisema kazi iliyofanywa na kampuni hiyo ni kuweka mgawanyo wa vyumba vya kuvalia nguo, vyoo na mabafu ya kuogea kwa kila timu, sambamba na vyumba vya waamuzi.
Alisema kuwa wameamua kuweka vyumba vya waamuzi, baada ya kuona wamekuwa wakihatarisha maisha yao kutoka kwa mashabiki, kwani awali walikuwa wakilazimika kupita karibu yao kipindi cha mapumziko na wakati mchezo umemalizika.
Aliongeza kuwa, kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na wamiliki wa uwanja ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kuanza kutengeneza sehemu ya kuchezea (pitch), na sasa kukarabati vyoo ni mwanzo wa mashabiki na wakazi wa Mbeya kupata mechi nyingi za kimataifa, wakianza na mchezo wa Taifa Stars na Malawi, kutokana na uwanja huo kuwa na vigezo vya  kimataifa.
“Kwa kweli kuna mabadiliko makubwa katika uwanja wetu na naipongeza Kampuni ya Mayuma, kwani imefanya kazi vizuri licha ya kuwa ilikuwa ngumu na imani yangu ni kuwa TFF itawaangalia watu wa mkoa huu na kuwaunga mkono watu wa Mbeya kwa kuwapa michezo mingi ya kimataifa,” alisema Mwaluka na kuongeza:
Kuhusu gharama zilizotumika kwa ajili ukarabati huo, Mwaluka alisema kuwa awali bajeti ilikuwa ni sh milioni 5, lakini kutokana na ugumu wa kazi hiyo huenda zikaongeza hadi kufikia milioni 8 hadi kukamilika kwake.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mayuma, Kura Mayuma, alisema kuwa asilimia kubwa ya ujenzi pamoja na marekebisho ya uwanja huo yameshakamika kwa asilimia 95 na kazi iliyosalia ni ndogo, ambako ndani ya siku mbili vyoo hivyo vitakuwa vimekamilika.
Mayuma aliongeza kuwa, kazi hiyo imechukua muda mrefu kumalizika kutokana na kuchelewa kuingia mkataba na wamiliki wa uwanja, vinginevyo ungekuwa umeishakamika
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

Post a Comment