Azam FC yawaita Yanga ili kumjadili Sure boy
Uongozi wa Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC, umewataka Yanga kwenda kufanya mazungumzo kama wanamuhitaji kiungo wao, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, kwani bado wana mkataba naye.Yanga wamefikia hatua ya kumuhitaji Sure Boy, wakiwa na lengo la kulipiza kisasi cha kuchukuliwa kwa kiungo wao mahairi, Frank Domayo ‘Chumvi’ na mshambuliaji Didier Kavumbagu.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Azam FC jana zinaeleza kuwa, wao hawana shaka wala chuki na Yanga, hivyo kama wanamuhitaji Sure Boy waende mezani wazungumze, kwani wanathamini wachezaji wao, hivyo hawawezi kumuachia aondoke kirahisi.
Chanzo hicho kilisema kuwa, wanatambua Sure Boy ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo hapa nchini, ila hawatasita kuwapa Yanga kama wataweza kutimiza masharti ambayo watawapa.
“Taarifa za Yanga kumtaka Sure Boy tumezisikia, lakini kama wanamtaka waje kwetu viongozi tuzungumze, kwani sisi hatuna shaka wala wasiwasi katika hili, tukimalizana tunawapa lakini wasijefanya kinyume na hapo, bado ana mkataba,” alisema Kiongozi huyo ambaye hakuna jina lake kuandikwa kwa madai sio msemaji wa timu hiyo.
Hata hivyo habari kutoka Yanga zinasema kuwa, aliyekuwa kocha wa Yanga, Hans Paluijm katika ripoti yake alimtaka kiungo huyo ambaye atasaidia safu hiyo iliyoonekana kupwaya katika ligi iliyopita.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:
Post a Comment