Friday, 16 May 2014

Tuko kamili kupambana na Zimbabwe-Nooij



KOCHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mart Nooij amesema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mechi ya Kombe la Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (Mei 16 mwaka huu), Nooij amesema kabla ya kuja Tanzania alikuwa akifuatilia Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), hivyo anawafahamu wachezaji wengi.

Amesema wachezaji wanaounda kikosi chake ni wenye uzoefu na mechi za kimataifa, hivyo wapo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani wamepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyokuwa Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Nooij amesema ujio wa washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (RDC) kutaongeza morali ya kikosi chake.
Samata na Ulimwengu watawasili nchini Jumamosi mchana, saa 7.30 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo leo (Mei 16 mwaka huu) wanacheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Al Hilal ya huko.

Wachezaji waliopo kambini kwa sasa ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Said Moradi, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Nadir Haroub, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Himid Mao, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Amri Kiemba, Jonas Mkude, Haruna Chanongo, Simon Msuva, Mrisho Ngasa, Khamis Mcha, Ramadhan Singano, John Bocco, Elias maguli na Kelvin Friday.

0 comments:

Post a Comment