Tuesday, 10 June 2014

Kipa Friedel asaini Spurs,sasa kuvunja rekodi huko Uingereza.

Klabu ya Tottenham  Hotspur imemuongezea Mkataba wa Mwaka Mmoja Kipa wao Brad Friedel na sasa yupo njiani kuvunja Rekodi ya Mchezaji mwenye Umri mkubwa kuchezea Ligi Kuu Uingereza.
Friedel, mwenye Miaka 43, ataivunja Rekodi inayoshikiliwa na John Burridge wa Manchester City ambaye Mwezi Mei 1995 alicheza dhidi ya Queens Park Rangers akiwa na Umri wa Miaka 43 na Siku 162.
Kipa huyo Mmarekani alihamia Tottenham Julai 2011 kutoka Aston Villa kwa Uhamisho Huru na amekuwa akitumika kama chaguo la pili kwa Hugo Lloris ambae ni Kipa Nambari moja wa Ufaransa.
Msimu uliopita, Brad Friedel alidakia Mechi moja ya Ligi na Msimu huu mpya unaokuja Spurs inataka kumtumia hasa kama Balozi wao huko Marekani lakini anaweza kuja kuitwa ili adake na hivyo anaweza kuivunja Rekodi ya Mchezaji Mzee kwenye Ligi Kuu Uingereza.
Friedel amecheza Ligi Kuu Uingereza kwa Miaka 17 akidakia Klabu za Liverpool, Blackburn Rovers na Aston Villa kabla kuhamia Spurs ambako amecheza mara 67.
Pia ameidakia Nchi yake ya Marekani  mara 82 na kucheza Fainali za Kombe la Dunia mara mbili.

0 comments:

Post a Comment