Luis Suarez afunguliwa mashitaka na FIFA
FIFA imefungua Mashitaka dhidi ya mshambuliaji wa Uruguay Luis Suarez baada kuonekana akimng’ata Meno Beki wa Italia Giorgio Chiellini kwenye Mechi ya Kombe la Dunia iliyochezwa Jana huko Brazil.
Suarez, mwenye
Miaka 27, pamoja na Chama cha Soka cha Uruguay wamepewa hadi Leo Saa 5
Usiku, Saa za Tanzania ili kujibu Mashitaka hayo.
Suarez alimvaa Chiellini, muda mfupi kabla Uruguay hawajafunga Bao lao la ushindi, na kuonekana akimuuma Beki huyo wa Italia ila mwamuzi hakuchukua hatua yeyote wakati huo.
Ikiwa Suarez atapatikana na hatia, Adhabu ya juu kabisa ambayo FIFA inaweza kumpa ni kumfungia Mechi 24 au Miaka Miwili.
Akijitetea baada ya Mechi wakati
akiongea na Kituo cha TV cha Uruguay, Suarez alisema: “Hivi vitu
vinatokea Uwanjani. Tulikuwa sisi wawili kwenye Boksi na yeye akanigonga
na Bega. Haya yanatokea Uwanjani, na vitu visikuzwe!”
Chiellini amemweleza Suarez kama ‘mwizi’
na kusema: “Ningependa kuona kama FIFA wana uhodari wa kuchukua
ushahidi wa Video dhidi yake. mwamuzi aliona alama za Meno lakini hakufanya
lolote!”
Mara baada ya tukio hilo, Suarez alijiangusha na kushika mdomo wake akijidai alipigwa kiwiko mdomoni.
Chiellini alimkimbilia mwamuzi kutoka
Mexico, Marco Rodriguez, na kuvua Jezi yake akimwonyesha Bega la Kushoto
lililoumwa Meno na wakati akifanya hivyo Fowadi wa Uruguay Gaston
Ramirez alijaribu kumzuia kwa kuipandisha Jezi ya Chiellini izibe Bega
lake.
Dakika chache baada ya mkasa huo Diego
Godin alifunga Bao la Kichwa, Dakika ya 81, na kuipa Uruguay ushindi wa
Bao 1-0 na kutinga Raundi ya Pili ya Kombe la Dunia na kuiacha Italy,
waliowahi kuwa Mabingwa wa Dunia mara 4 na waliotaka Sare tu, kuaga
Mashindano.
Ikumbukwe kuwa Aprili 2013, Luis Suarez alifungiwa
Mechi 10 kwa kumuuma Meno Beki wa Chelsea Branislav Ivanovic kwenye
Mechi ya Ligi Kuu England.
Isitoshe Mwaka 2010 huko Uholanzi, Suarez alifungiwa Mechi 7 kwa kumuuma Kiungo wa PSV Eindhoven Otman Bakkal.
Miaka minne iliyopita huko Afrika Kusini
kwenye Fainali za Kombe la Dunia Suarez alizuia Mpira uliokuwa ukitinga
Golini kwenye Dakika ya 120 kwa Mkono wake na yeye kutolewa nje kwa
Kadi Nyekundu, Ghana kupewa Penati ambayo Asamoah Gyan aliikosa na
hatimaye Uruguay kutinga Nusu Fainali kwa Mikwaju ya Penati.
0 comments:
Post a Comment