RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MWANAKATWE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe kilichotokea jana asubuhi (Juni 7 mwaka huu) katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba
yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa
katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati
madaktari wakimpatia matibabu.
Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa
Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi
uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.
Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika
kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwen enzi za uhai wake alitoa mchango
mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna wa CAF.
TFF inatoa pole
kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Wananchi
wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika
kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa
na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na hoteli ya Giraffe
wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF tunasubiri taratibu hizo
ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.

0 comments:
Post a Comment