Azam yaimwagia fedha timu ya Madola
Kampuni ya Azam jana ilitoa kiasi cha dola 93,000 za Marekani kwa timu ya taifa inayokwenda Glasgow, Scotland kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola.Fedha hizo zilizokabidhiwa jana kwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma Nkamia, ni kwa timu hiyo inayoundwa na nyota wa ndondi, kuogelea, baiskeli, riadha, judo na uzito.
Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Waziri Nkamia, aliishukuru Kampuni ya Azam kwa sapoti hiyo akisema itasadia timu hiyo kwa hali na mali.
Nkamia alifungua milango zaidi kwa makampuni, mashirika na taasisi mbalimbali nchini kuisaidia timu hiyo ili wachezaji waweze kufanya vizuri katika mashindano hayo yatakayoanza Julai 23.
“Tunawashukuru sana Azam, maana jana (juzi) rais aliniambia juu ya hili suala, leo (jana) tunaona wamekuja kutusapoti, tunashukuru sana,” alisema Nkamia na kuongeza hata yeye ataungana na wachezaji hao nchini Scotland.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Azam, Said Mohamed, alisema wamelazimika kurejesha kiasi kidogo kwa Watanzania ambao ni wateja wao wakubwa.
“Tumetoa kiasi hiki kama ishara ya kurejesha fadhila kwa Watanzania ambao wamekuwa wakituunga mkono katika bidhaa zetu, tuko nyuma yao,” alisema.
Katika hatua nyingine, Nkamia alisema wizara yake imepanga kuzungumza na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutoa fursa kwa timu kuutumia Uwanja wa Azam Complex, ulioko Chamazi kwa mechi za usiku.
“Tutaongea na ndugu zetu TFF waweze kutoa nafasi kwa timu kucheza usiku katika Uwanja wa Azam kwani una vigezo vyote katika kuzipa timu uzoefu wa kucheza usiku,” alisema Nkamia.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment