Wednesday, 16 July 2014

Ingawa ametwaa ubingwa mara tatu mfululizo na Juventus,Conte ajiuzulu.

Kocha Antonio Conte wa Mabingwa wa Serie A huko Italia, Juventus, ameacha kazi yake kwa makubaliano ya pande zote mbili.
Conte, ambaye aliwahi kuwa Nahodha wa Juventus enzi za uchezaji wake, ameiongoza Juventus kutwaa Ubingwa mara 3 mfululizo hadi sasa pamoja na kutwaa Supercoppa Italiana mara mbili mfululizo.
Mwezi Mei, Conte aliongeza Mkataba wake na Juve na ulitakiwa umalizike Mwaka 2015.
Lakini  Klabu hiyo imethibitisha kuwa wamekubaliana na Conte kuwa aondoke huku mwenyewe akidai amechoshwa na mafanikio ya Juventus.
Conte, ambaye pia ni Mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Italia, anahusishwa sana na kutwaa wadhifa aliouacha Cesare Prandelli wa kuifundisha Timu ya Taifa ya Italy. Prandelli alijiuzulu mara tu baada ya Italia kushindwa kufuzu kutoka Kundi D la Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil.
Hivi sasa Prandelli amejiunga na Galatasaray ya Uturuki kama Meneja wao mpya.
Lakini kuhusu kuwa Meneja wa Italia Conte amekanusha kwa kusema: “Mimi naishi wakati wa sasa, nafikiria uamuzi huu niliochukua!”
Hivi karibuni Juventus imekumbwa na vuta nikuvute huku Wachezaji wao Mastaa wakihusishwa na kuihama kwa Arturo Vidal kuhusishwa na Manchester United na Paul Pogba kukimbizwa na Chelsea.

0 comments:

Post a Comment