Samata na Ulimwengu watua nchini tayari kuwavaa Msumbiji.
Nyota tegemeo wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wamewasili Dar es Salaam asubuhi ya leo kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya mchezo wa kimataifa dhidi ya Msumbiji ‘Mambas’ mwishoni mwa wiki.Washambuliaji hao wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wote wamewasili wakiwa fiti tayari kwa mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Pili na ya mwisho kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Morocco.
Mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, wachezaji hao walisema kwamba wanashukuru wameruhusiwa mapema kuja kujiunga na Stars kwa ajili ya mchezo huo wa Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika (AFCON) itachezwa Jumapili (Julai 20 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Nyota hao walitokea Tunisia ambapo timu yao ya TP Mazembe imepiga kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imepiga kambi Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mahmoud Ashour kutoka Misri.
Stars itarejea jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa (Julai 18 mwaka huu) kwa ajili ya mechi hiyo wakati Mambas nao wanatarajiwa kutua siku hiyo hiyo.
Mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti 1 na 3 mwaka huu nchini Msumbiji.
0 comments:
Post a Comment