Thursday, 3 July 2014

Logarusic ataka wiki sita kunoa Simba

Klabu ya Simba chini ya uongozi mpya wa Rais Evance Aveva, umetamka rasmi kumbakisha kocha wao Mcroatia, Zdravko Logarusic ‘Loga’ katika kuipa makali timu hiyo.
Akithibitisha hilo jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga, alisema kwa mujibu wa programu ya kocha huyo, ametaka kambi ya wiki sita kabla ya kuanza Ligi Kuu Tanzania bara.
Alisema kwa vile ni programu ya kitaalamu katika kujenga kikosi bora cha ushindani, itatekelezwa kama ilivyo kwa maslahi ya timu hiyo iliyoshindwa kucheza michuano ya kimataifa kwa msimu wa pili mfululizo.
Ezekiel alisema baada ya kuwasiliana na Loga kwa njia ya simu, kocha huyo alisema muda huo ndio utatosha kuwapa makali vijana wake kabla ya kuanza kwa kampeni ya Ligi Kuu.
Alisema kutokana na mapendekezo hayo na mambo mengineyo muhimu, jana Kamati ya Utendaji ilikutana kuanza kusuka mipango.
“Kocha alipendekeza mazoezi yawe ya wiki sita kabla ya kuanza ligi, hivyo Kamati ya Utendaji inatarajiwa kukutana leo jioni (jana) kuangalia jinsi ya kuisuka timu na ujio wa kocha ambaye yupo kwao Croatia kwa mapumziko,” alisema.
Alisema uongozi umekubaliana na wazo hilo, wakiamini kama litatekelezwa, timu hiyo itatisha msimu huu.
Ligi Kuu imepangwa kuanza Agosti mwaka huu, huku Simba ikitaka kufuta makosa ya kumaliza nafasi ya tatu na nne katika misimu miwili iliyopita.
Chanzo;Tanzania Daima.

0 comments:

Post a Comment