Makundi ya kombe la Kagame 2014 yapangwa.
Yanga SC imepangwa Kundi A katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame pamoja na wenyeji, Rayon Sport, Coffee ya Ethiopia, Atlabara ya Sudan Kusini na KMKM ya Zanzibar.Katika droo iliyopangwa jana mjini Kigali, Rwanda chini ya Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, Kundi B lina timu za APR ya Rwanda, KCC ya Uganda, Flambeau de L’Est ya Burundi, Gor Mahia ya Kenya na Telecom ya Djibouti.
Kundi C linaongozwa na mabingwa watetezi, Vital’O ya Burundi, El Merreikh ya Sudan, Polisi ya Rwanda na Benadir ya Somalia.
Droo ya michuano ya 40 ya CECAFA –Kagame ilihudhuriwa pia na viongozi wakuu wa Serikali ya Rwanda mjini Kigali
Timu 14 zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo kuanzia Agosti 8 hadi 24 mwaka huu- jumla ya mechi 34 zikichezwa katika viwanja vya Amahoro na Nyamirambo, Kigali.
Rais Paul Kagame wa Rwanda ndiye mlezi wa mashindano haya ambaye hutoa dola za Kimarekani 60,000 kila mwaka kwa ajili ya zawadi.
Wizara ya Michezo ya Rwanda na mashirika mengine yatadhamini michuano hiyo, itakayokwenda sambamba na maazimisho ya miaka 20 ya mauwaji ya kimbali.
Televisheni ya kulipia ya Supersport ya Afrika Kusini ambao ni maswahiba wa muda mrefu wa CECAFA, ni miongoni mwa wadhamini pia na wataonyesha mechi zote za michuano hiyo moja kwa moja. Ratiba ya mashindano hayo inatarajiwa kutolewa wiki ijayo.
0 comments:
Post a Comment