Thursday, 3 July 2014

Washauri wa FIFA na pendekezo la wachezaji wanne wa akiba.

Jopo la Washauri wa Masuala ya Makocha la Shirikisho la soka Ulimwenguni FIFA  linatafakari kutoa mapendekezo kwa FIFA kuruhusu idadi ya Wachezaji wa Akiba wanaotoka Benchi na kuruhusiwa kucheza iwe Wanne badala ya Watatu wa sasa.
Lakini Jopo hilo linataka Mchezaji huyo wa Nne atakaeruhusiwa awe anaingizwa wakati wa Nyongeza za Dakika 30 baada ya Timu kwenda Sare katika Dakika 90.
Mmoja wa Wajumbe wa Jopo hilo Kocha wa zamani wa Liverpool, Gerard Houllier amesema: “Ni wazo zuri ambalo tutalipeleka kwenye Vikao vya Kutunga Sheria FIFA!”
Houllier, ambae pia aliwahi kuwa Kocha wa Ufaransa, amefafanua kuwa kuruhusu Mchezaji wa 4 kuingia kwenye Dakika za Nyongeza 30 itasaidia kupunguza athari za Wachezaji kubanwa na Msuli wakati huo na kuzipa nafuu Timu.
Aidha Houllier amesisitiza Wachezaji wanaotoka Benchi wana mchango mkubwa wa kubadilisha matokeo ya Mechi kwani huko Brazil kwenye Fainali za Kombe la Dunia Wachezaji waliotoka Benchi na kuingizwa wamefunga mabao 29 na kuvunja Rekodi ya Fainali za Kombe la Dunia za Mwaka 2006 huko Ujerumani walipofunga mabao 23 na bado  Mechi 8 hazijachezwa.
Houllier amesema: “Wachezaji wa Akiba wana umuhimu mkubwa kwa sababu wanaingia wakiwa na  akili mpya. Karibu robo ya Magoli yamefungwa kwenye Robo Saa ya mwisho huko Brazil. ”
Baadhi ya Magoli hayo ni mchango wa Klaas-Jan Huntelaar alipoingizwa Dakika ya 76 kutoka Benchi na kuisaidia Uholanzi  kwa kumpasia Wesley Sneijder Dakika ya 88 na kusawazisha na kisha yeye mwenyewe kufunga Bao la Pili na la ushindi kwa Penati ya Dakika ya 94 walipoibwaga Mexico 2-1.
Naye Kipa wa Marekani Tim Howard kuizuia Ubelgiji na kutoka suluhu katika Dakika 90, akaingizwa Romelu Lukaku ambaye, katika Dakika za Nyongeza 30, alimpasia Kevin De Bruyne aliyefunga Bao la kwanza na yeye mwenyewe kupiga Bao la pili na Ubelgiji kushinda  2-1.
Mwaka 2012, FIFA iliwahi kuyakataa mapendekezo ya aina hii hii ya kuongeza Wachezaji wa Akiba kuruhusiwa kucheza kuwa Wanne lakini safari hii Houllier anaamini yatapitishwa.

0 comments:

Post a Comment