Kabange ampongeza Mandawa kuwa mchezaji bora mwezi Novemba.
Kocha msaidizi wa Kagera Sugar Mrange Kabange amempongeza Mshambuliaji wa timu hiyo Rashid Mandawa baada ya kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kwa mwezi Novemba mwaka huu.Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF jana ilimtangaza Mandawa na atazawadiwa kitita cha sh. milioni moja.
Akizungumza na Sports4lifeTz akiwa mkoani Kagera,Kabange amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya Mandawa kuwa mchezaji bora mwezi Novemba.
Kocha huyo amesema kuwa Baada ya kuondoka kwa Themi Felix aliyetimkia Mbeya City walipata wakati mgumu wa kuziba nafasi hiyo ila baada ya Mandawa kuonesha kiwango kizuri pengo la Felix limezibwa vema.
Mandawa ambaye kwa mwezi huo alichuana kwa karibu na mshambuliaji Fulgence Maganda wa Mgambo Shooting ya Tanga na nahodha wa Simba, Joseph Owino atakabidhiwa zawadi yake na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Vodacom.
Hafla ya kukabidhi zawadi hiyo inatarajiwa kufanyika wakati wa mechi ya raundi ya nane ya ligi hiyo kati ya Simba na Kagera Sugar itakayochezwa Desemba 26 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

0 comments:
Post a Comment