Haruna Chanongo afungiwa Mechi tatu,huku FDL faini yatolewa kwa timu za Polisi.
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB)
imewapiga faini na kuwafungia mechi
wachezaji wawili wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
kwa kufanya vitendo kinyume na kanuni zinazotawala ligi hizo.
Taarifa ya TFF iliyotumwa katika mtandao huu ni kwamba Mshambuliaji Haruna Chanongo wa Stand
United amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kwa kumpiga teke
mwamuzi wa mechi dhidi ya Polisi Morogoro iliyochezwa Januari 3 mwaka huu
Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni
ya 37(3) ya Ligi Kuu.
Kipa Amani Simba wa Oljoro JKT amepigwa
faini ya sh. 300,000 kwa kukataa kupeana mkono na viongozi wakati wa kusalimia
kabla ya kuanza mechi kati ya timu yake na Toto Africans iliyofanyika jijini
Mwanza. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 14 ya FDL.
Timu ya Polisi Mara imepigwa faini ya
sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki wake wakati wa mechi ya FDL dhidi
ya Mwadui ya Shinyanga iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Pia Polisi Tabora imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na vurugu za washabiki
wake kwenye mechi namba 40 dhidi ya Geita Gold, adhabu ambazo zimetolewa kwa
mujibu wa kanuni ya 41.

0 comments:
Post a Comment