Fainali Beach Soccer kuchezwa leo
Fainali ya michuano ya mpira wa miguu ya
ufukweni (beach soccer) kati ya timu za Taasisi ya Teknolojia Dar es
Salaam (DIT) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) inachezwa leo (Mei 25
mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni jijini Dar es
Salaam.
Timu hizo zimepata nafasi ya kucheza
fainali baada ya kushinda mechi zao za nusu fainali dhidi Chuo Kikuu cha
Ardhi (AU) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) zilizochezwa wikiendi
iliyopita.
Mgeni rasmi katika fainali hiyo
itakayooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Azam Tv
atakuwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal
Malinzi na itaanza saa 4.15 asubuhi. Fainali hiyo itatanguliwa na mechi
ya kutafuta mshindi wa tatu kati ya AU na TIA kuanzia saa 3 kamili
asubuhi.
Michuano hiyo ambayo ni ya kwanza
kufanyika nchini ilishirikisha vyuo 13 vya Dar es Salaam, na ilianza
Aprili 20 mwaka huu katika fukwe za Escape One na Gorilla iliyopo
Kigamboni.
Vyuo vingine vilivyoshiriki ni Chuo
Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es
Salaam (TUDARCO), Taasisi ya Ustawi wa Jamii (ISW) na Chuo cha
Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma
Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Utawala wa Kodi
(ITA), Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Uandishi wa
Habari Dar es Salaam (DSJ).
Tanzania itashiriki katika michuano ya Afrika ya mpira wa miguu wa ufukweni itakayofanyika mwakani nchini Shelisheli.
0 comments:
Post a Comment