Wednesday, 21 May 2014

Mbeya city bado wapo Dar michuano kuanza kesho

MICHUANO mipya ya CECAFA Nile Basin Cup inatarajia kuanza kutimua vumbi hapo kesho (juni 22) mwaka huu, lakini wawakilishi wa Tanzania, Mbeya City fc mpaka leo hii wapo jijini Dar es salaam, huku hatima yao ikiwa matatani.
Musa Mapunda, mwenyekiti wa Mbeya City fc ameeleza  kuwa mpaka usiku huu hawajapata tiketi za safari hiyo na mbaya zaidi hakuna mawasiliano yoyote kutoka CECAFA wala TFF.
“Tupo Dar es salaam mpaka sasa. Michuano inaanza kesho. Tungejua tusingeihamisha timu Mbeya. Tunatumia gharama zetu hapa Dar. Ni hasara kubwa kwa klabu”. Alisema Mapunda.
Chama cha soka nchini Sudan kwa kushirikiana na serikali ndio wadhamini wa mashindano hayo na wao ndio wanaobeba gharama zote.
Mbeya city fc wanatarajia kuanza kampeni zao juni 23 mwaka huu dhidi ya El Mereikh ya Sudan.
Hata hivyo walihitaji kuondoka juzi ili angalau kupata siku mbili tatu kwa ajili ya kuzoea hali ya hewa ya Sudan ambayo ni joto sana.
Wachezaji wa klabu hiyo wamezoea ubaridi wa Mbeya, hivyo mazingira ya Sudan yatakuwa mapya kwao na ndio maana walihitaji kwenda mapema.
Kwasasa kikosi cha Mbeya City kinaendelea na mazoezi yake katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Maka Mwalwiysi amesema kwa asilimia kubwa kikosi kipo salama na wachezaji wapo katika morali kubwa.
“Tumeshaiandaa timu vizuri na kinachosubiriwa ni kukamilika kwa taratibu za safari. Ni michuano mizuri kwetu na tunaamini tutafanya vizuri licha ya uchanga wetu”. Alisema Maka
Chanzo:Shafih dauda in sports

0 comments:

Post a Comment