TFF kuanzisha mfuko wa maendeleo,mwenyekiti ni Tenga.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeazimia
kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania (TFF Development Trust
Fund).
Uamuzi wa kuanzisha mfuko huo umepitishwa katika kikao
cha Kamati ya Utendaji ya TFF iliyokutana Mei 3 mwaka huu jijini Dar es Salaam
ambapo madhumuni yake ni kutafuta vyanzo vya rasilimali za kuendeleza programu
za mpira wa miguu Tanzania.
Mfuko huo utakaokuwa chini ya uenyekiti wa Rais
aliyepita wa TFF, Leodegar Tenga utatafuta rasilimali za kuendeshea michuano ya
Taifa na kimataifa ya wavulana na wasichana kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 13, 15, 17 na 19.
Pia kuendeleza maeneo ya ardhi kote Tanzania ambayo ni
mali ya TFF kwa kujenga vituo vya michezo (sports centres), kutafuta rasilimali
za kutoa mafunzo kwa makocha, marefa, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi
(administrators).
Majukumu mengine ya mfuko huo ni kuagiza na kusambaza
vifaa vya michezo hasa kwa watoto wadogo (grassroots) na vijana.
Mfuko huo utazinduliwa Oktoba 8 mwaka huu ambayo ni
siku ya kilele cha Tanzania kutimiza miaka 50 ya uanachama wake katika
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
Mbali ya Tenga, wajumbe wengine wanaounda bodi ya mfuko
huo ni Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ayoub Chamshama, Katibu Mkuu wa zamani wa
TFF, Fredrick Mwakalebela, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha,
Tarimba Abbas na Mbunge wa Viti Maalum, Zarina Madabida.
0 comments:
Post a Comment