Baada ya kuitoa Zimbabwe,Taifa stars kutua nchini leo
Kikosi cha Taifa Stars ambacho
jana (Juni 1 mwaka huu) kiliitupa Zimbabwe (Mighty Warriors) nje ya
michuano ya Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 kinarejea nchini
leo (Juni 2 mwaka huu) kutoka Harare.
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa 12.30 jioni kwa ndege ya Kenya
Airways ikitokea Harare kupitia Nairobi.
Stars imefuzu kucheza raundi
inayofuata kwa ushindi wa jumla ya mabao 3-2, kwani awali (Mei 18 mwaka
huu) iliifunga Zimbabwe bao 1-0 katika mechi ya kwanza iliyochezwa
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika raundi ya pili, Taifa
Stars itacheza na Msumbiji ambapo itaanzia nyumbani kati ya Julai 19 na
20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya
Agosti 2 na 3 mwaka huu.
Wakati huo huo, Taifa Stars
imeendelea kupokea salamu za pongezi kutoka kwa wadau mbalimbali baada
ya kufanikiwa kuvuka kikwazo hicho cha kwanza katika harakati zake za
kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Salamu hizo zimetoka kwa Chama
cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Manyara (MARFA), mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) akiwakilisha Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Mwanza (MZFA), John Kadutu, na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ahmed Idd Mgoyi.
0 comments:
Post a Comment