Tuesday, 17 June 2014

Sina chuki na Wambura bali maamuzi ya kamati-Ndumbaro.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Wakili Dk Damas Ndumbaro amesema kwamba uamuzi wowote dhidi ya mgombea Urais wa klabu hiyo, Michael Richard Wambura hautokani na chuki binafsi.
Dk Ndumbaro kwamba, hakuna msuguano wowote, baina yake na Wambura na maamuzi yote yanayomuumiza mgombea huyo, si yake binafsi, bali ya Kamati.
Ikumbukwe Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC ilimuengua Wambura kwa sababu alikiuka Katiba kwa kuipeleka klabu hiyo Mahakamani, jambo ambalo FIFA inakataza.
Wambura alikata rufaa, Kamati ya Rufani ya TFF chini ya Mwenyekiti Wakili Julius Lugaziya, ambako alishinda na kurejeshwa kwenye kinyang’anyiro.
Wakili Lugaziya alisema Kamati yake iliamua kumrejesha Wambura kwa sababu baada ya kosa alilolifanya aliendelea kuhudhuria mikutano ya klabu, kulipia ada zake za uanachama na pia akateuliwa katika Kamati ya Utendaji, iliyounda Kamati ya Uchaguzi ya sasa chini ya Ndumbaro.  
Lakini jana, Ndumbaro baada ya ripoti ya Wakili Lugayiza alisema amemuengua tena Wambura kwa sababu amekiuka kanuni za uchaguzi kwa kufanya kampeni kabla ya muda.
Huku kukiwa  kuna wasiwasi, Mwenyekiti wa klabu ya Simba SC Ismail Aden Rage anaweza kuivunja Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo,Ndumbaro amesema hilo haliwezekani.
Wakili Ndumbaro amesema kwamba kwa mujibu wa Katiba ya Simba SC, baada ya kuundwa kwa Kamati ya Uchaguzi inapaswa kufanya kazi kwa miaka miwili.
Wakili Ndumbaro amesema kwamba Kamati hiyo inaweza kuvunjwa kabla ya kufikisha muda huo, iwapo itabainika imefanya makosa na wenye uwezo wa kuivunja ni Mkutano Mkuu wa wanachama wa klabu
“Rage hana uwezo wa kuivunja Kamati yetu hadi baada ya miaka miwili tangu iundwe,”amesema Ndumbaro na alipoulizwa iwapo itabainika Kamati ilifanya makosa katika utendaji wake, alijibu; “Hapo sasa ni Mkutano Mkuu ndiyo unaoweza kutuondoa sisi hapa,”.
Chanzo;Binzubeiry

0 comments:

Post a Comment