Kagame kuanza Agosti 9 nchini Rwanda
![]() |
| Kikosi cha Vital ' O kilichobeba ubingwa 2013 |
Akizungumzia hilo Katibu Mkuu wa CECAFA,
Nicholas Musonye amesema Mechi zote zitachezwa Mjini Kigali kwenye Viwanja vya
Amahoro na Nyamirambo huku Rubavu ikiwa ni Uwanja wa Akiba.
Vilevile Musonye amesifu
Shirikisho la Soka la Rwanda, FERWAFA, na Wizara ya Michezo na Utamaduni
ya Rwanda kwa kutoa ushirikiano mzuri na kuandaa mipango mizuri.
Musonye alikumbusha kuwa mara ya mwisho
kwa Kagame Cup kufanyika Nchini Rwanda ilikuwa Mwaka 2010 na yalifana
sana na kuwa na mafanikio makubwa.
Klabu 4 kutoka Angola, Congo DR na Congo
Brazaville huenda zikaalikwa kushiriki michuano hiyo ambayo washiriki
wake wa kawaida ni Wanachama wa CECAFA na ambayo tangu Mwaka 2002
Mdhamini wake mkuu ni Rais Paul Kagame wa Rwanda ambae amekuwa akitoa
Dola 60,000 kila Mwaka.
Akiongea, Musonye alisema: “Rwanda iko
tayari, CECAFA iko tayari na Timu zetu zipo tayari kuja. Tutakuwa na
Timu nyingi kwa Mashindano haya kuliko nyuma.”
Musonye alitoa shukrani za dhati kwa Rais Kagame kwa msaada wake.
Vile vile, Musonye amedokeza kuwa
Klabu ya Uganda, Sports Club Victoria University, iliyotwaa CECAFA Nile
Basin Cup huko Sudan Mwezi uliopita, na AFC Leopards ya Kenya, huenda
zikaalikwa kwa kuonyesha ushindani mzuri kwenye Nile Basin Cup ambayo
yalikuwa Mashindano mapya ya CECAFA.
Klabu Vigogo za Afrika Mashariki na
Kati ambazo zitakuwepo huko Rwanda ni pamoja na KCCA FC ya Uganda, Gor
Mahia ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda, Yanga ya Tanzania na Mabingwa
Watetezi Vital ‘O kutoka Burundi iliyotwaa Kombe huko Darfur, Sudan
Mwaka Jana baada kuibwaga APR ya Rwanda 2-0 kwenye Fainali.
Mashindano haya yatarushwa moja kwa moja kwenye TV na SuperSport International.
Ratiba kamili itatolewa baadae na CECAFA baada Timu zote kuthibitisha kushiriki.
Mbali ya kutwaa Kombe, Bingwa wa Kagame
Cup huzoa Donge la Dola 30,000, Mshindi wa Pili Dola 20,000 na Timu ya
Tatu hupata Dola 10,000.

0 comments:
Post a Comment