Monday, 14 July 2014

Kushuhudia Serengeti boys na Afrika kusini 2000/-


Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetangaza viingilio vya mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika kwa vijana wa chini ya miaka 17 kati ya Tanzania ‘Serengeti Boys’ na Afrika Kusini ‘Amajimbos’ ambapo kiingilio kitakuwa sh  2,000.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, mechi hiyo itachezwa Julai 18, katika Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 9.
Kuhusu waamuzi, alisema ni kutoka Shelisheli ambapo mwamuzi wa kati ni Allister Barra atakayesaidiwa na Gerard Pool, Jean Joseph na Felix Ernest huku mwamuzi wa mezani atakuwa Nelson Emile Fred.
Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Andriamiasasoa Doda Nirimboavonjy kutoka nchini Madagascar.
Alisema, kikosi cha Serengeti Boys chini ya kocha Hababuu Ali Omari kipo kambini kwa zaidi ya wiki mbili kikijiandaa kwa mechi hiyo ambapo mechi ya marudiano itachezwa kati ya Agosti Mosi na 3 nchini Afrika Kusini.
Aidha, Alfred Kishongole Rwiza wa Tanzania ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya marudiano ya michuano hiyo ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Rwanda na Uganda.

0 comments:

Post a Comment