Mpombo Cup kuanza kutimua vumbi kule Singida.
Mashindano yaliyopewa jina la “Mpombo Cup 2014” katika jimbo la Singida Kaskazini yameanza kutimua vumbi kwenye viwanja 38 katika wilaya ya Singida vilivyotengwa kwa ajili ya mashindano hayo.Mashindano hayo yaliyotanguliwa na Kauli Mbiu isemayo “Tushiriki kuibua vipaji,Singida Kaskazini yanalenga kukuza pamoja na kuleta maendeleo ya michezo na utamaduni,hususani katika jimbo la Singida Kaskazini.
Mwenyekiti wa mashindano hayo,Michael Athumani Mpombo amebainisha hayo alipokuwa akisoma risala fupi kwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa mashindano ya Mpombo Cup 2014 uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mgori,katika jimbo la Singida kaskazini.
Aidha Mpombo ambaye pia ni muandaaji wa mashindano haya amefafanua kwamba mashindano hayo yatakayogharimu jumla ya fedha za kitanzania shilingi milioni thelathini hadi kufikia fainali zake,yatashirikisha jumla ya timu 83.
Hata hivyo muandaaji huyo ameweka bayana kwamba Programu hiyo ya Mpombo Cup ya mwaka 2014 itakuwa chini ya familia ya Mpombo kwa kushirikiana na Chama cha mpira wa miguu cha Wilaya ya Singida Vijijini (SIRUFA) kwa ujumla wake katika hatua zake zote za uanzishwaji,utekelezwaji,usimamizi pamoja na tathimini.
Kuhusu zawadi za mashindano haya yatakayochezwa nyumbani na ugenini,mwenyekiti huyo amesema mshindi wa kwanza kwenye ngazi ya kata atakabidhiwa 250,000/=wakati mshindi wa kwanza kwenye ngazi ya tarafa atakabidhiwa 500,000/= na bingwa wa mashindano hayo atakabidhiwa shilingi milioni moja pamoja na kombe lenye thamani ya 250,000/=.
Kwa mujibu wa Mpombo mshindi wa pili atapata 500,000/=pamoja na medali ya fedha mshindi wa tatu 250,000/=medali ya shaba na mshindi wa nne 100,000/=.
Akifungua mashindano hayo,Katibu wa Chama cha mpira wa miguu(SIRUFA) Mkoa wa Singida,Hussein Mwamba ametumia fursa hiyo kukemea baadhi ya wanasiasa wanaopinga jitihada nzuri sana kwenye sekta ya michezo zinazonyeshwa na wadau kwa lengo la kuibua vipaji vya vijana.
Nao baadhi ya washabiki wa mchezo huo wa soka waliohojiwa na kituo hiki wamesema kutokana na mfano ulioonyeshwa na muandaaji wa mashindano haya,ufike wakati na watu wengine wakaiga uhamasishaji huo badala ya kuingiza siasa kwa lengo la kuhofia kunyang’anywa nafasi walizonazo na watu wasiokuwa hata na ndoto za kugombea nafasi za uongozi fulani.
0 comments:
Post a Comment